Abstract:
Tasfida ni matumizi ya lugha kwa ustadi unaopunguza makali ya
maneno yanayotumiwa. Ikiwa maneno au misemo hiyo ina dalili za
kutusi, kukirihi au kuweka maneno mwiko hadharani basi hutumiwa
lugha inayoficha sifa hizi mbaya zinazojulikana na jamii. Imejitokeza
katika mawanda ya matumizi ya neno ‘choo’ kuwa ni uchafu na hivo
wanafunzi wa shule za Msingi na Upili katika mitalaa yao huambiwa
wasilitumiye badala yake watumiye ‘msala’ au ‘haja’. Makala haya
yameonesha hata hilo neno ‘choo’ piya ni tasfida na lafaa kutumiwa
waziwazi katika maongezi ya kawaida. Kufikiya hatuwa hii,
tumebainisha matumizi ya maneno ‘choo’, ‘msala’ na ‘haja’ na piya
tuliangaziya usuli wa ‘choo’ kiisimu. Uchanganuzi wetu umebaini
kuwa neno ‘choo’ latokana na ‘kioo’ lenye maana ya sehemu ya
kuoga au kujinadhifisha na hata linapotumiwa kwa maana ya mavi au
kinyeshi bado piya ni neno fiche lenye tasfida. Tunahitimisha kuwa
kutokana na ‘usafi’ wake, neno ‘choo’ linaweza kutumiwa sawiya na
maneno ‘msala’ au ‘haja’ ambayo ni ya mkopo na yenye maana
tafauti na kule yalikokopwa.